JULIUS MTATIRO :NGELEJA NI SHUJAA WANGU.

Kaka yangu mpendwa William Ngeleja amefanya uamuzi wa kishujaa sana, ameamua kujitakasa kwa kurejesha fedha za wizi ambazo aliyempa alituibia huko nyuma na jambo hili lilishafanyiwa maamuzi na bunge lakini hayakutelezwa.

Hata hivyo namkumbusha Ngeleja, kwamba makosa ya JINAI hayafi milele. Ukiua mwaka 1970 halafu ukaombwa ujitokeze, ukakataa, halafu mwaka 2017 (miaka 47 baadaye) ukajitokeza na maburungutu ya pesa au roho na mwili wa mtu mwingine ili uwakabidhi ndugu wa mtu uliyemuua kwa maana ya kuwalipa fidia, vitu vyako vitapokelewa lakini havifuti jinai.

Ukiiba hela za walalahoi mwaka 1950, halafu miaka 67 baadaye ukajitokeza na hela mara milioni elfu moja ya zile ulizoiba, zinaweza kupokelewa kwa mbwembwe kubwa, lakini hiyo haifuti jinai. Hata kama leo ungelikuja na viwanda vyote vya MO na BAKHRESA na vya DANGOTE uwakabidhi uliowahi kuwaibia senti tano huko nyuma, hiyo haifuti JINAI!

Ukishatenda jinai (makosa ambayo humaanisha umeshindwa kuwa mwaminifu) kama hili la kina Ngeleja, wewe ni mtenda jinai na dunia yote sheria ziko VERY CLEAR, Jinai haijadiliwi, haitafutiwi ufumbuzi, haifanyiwi maridhiano. Jinai ni makosa yenye adhabu kwa mujibu wa Sheria na adhabu hizo hazina mjadala.

Kama tungelikuwa na SERIKALI serious na inayokata kotekote, baada ya PRESS CONFERENCE ya kaka yangu NGELEJA, ilipasa TAKUKURU wamsubirie geti la HABARI MAELEZO na asionekane hadharani hadi awe mahakamani, kama kina Rugemarila!

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ni juzi tu hapa alitumia ile SHERIA ya kikoloni, kibaguzi na ya kitumwa, akaamuru Halima Mdee akamatwe mara moja na kusota rumande, JUST BECAUSE Halima alizungumza na vyombo vya habari na akaonya juu ya mienendo ya Rais Magufuli.

Ni juzi pia wale viongozi karibu 50 wa CHADEMA waliokuwa kwenye kikao halali wa ndani huko Geita, walizingirwa na Polisi na kukamatwa kwa nguvu kubwa sana, kisa walikuwa wanatimiza haki yao ya kikatiba kama chama cha siasa.

Huwa najiuliza, hivi tuna dola ngapi Tanzania? Hivi tuna serikali zinazofanya kazi kwa kutumia sheria zipi kuhusu wale wa Geita au zipi kwa mbunge wa KAWE?

Godbless Lema alipotangaza ile ndoto yake. Aliishia gerezani miezi minne. Lakini Ngeleja ametangaza hadharani kuwa amerudisha fedha za wizi, hadi sasa yuko kwake! Are we kidding?

How could you arrest a person who predicted Ideal things which you are framing them to being against the LAW and leave free the one who said real things which are absolutely against the law? (Unawezaje kumshughulikia mtu aliyetabiri mambo ya kufikirika tu ambayo umeamua kuigiza kuwa mambo hayo ni kinyume na sheria, na wakati huohuo ukamuacha huru mtu ambaye ameeleza mambo halisi ambayo ni makosa ya jinai yasiyo na mjadala?)

Rugemalila pia ni Binadamu jamani, kama yeye yuko gerezani kwa sababu ya fedha alizoiba, vipi kuhusu wale waliopokea fedha hizo za wizi na tena wengine wakasema ni hela za mboga?

Kama Rugemalila yuko gerezani kwa kukwapua fedha za umma. Vipi wale watendaji na viongozi wa serikali na Benki Kuu ya Tanzania walioidhinisha fedha zile zitoroshwe BoT wako huru, mitaani? Yani unamkamataje mwizi aliyeiba fedha halafu wale waliomfungulia geti na kumhesabia fedha kwa hiyari na wale waliowatuma wakiwemo hadi watendaji wa ikulu, wako mitaani salama?

Unamshughulikiaje Rugemalila na kuwaacha watendaji wa Benki ya Stanbic na Benki ya Mkombozi ambao walizitumia benki zao kutakatishia fedha hizo bila kujali kuwa kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za fedha na sheria za nchi?

Tunakumbuka kuwa bunge liliazimia fedha zile zirejeshwe kwa kulipiwa kodi? Ilikuwa mwaka 2014, kina Ngeleja hawakurudisha fedha hizo, kina Chenge, Askofu wangu Kilaini n.k. waliendelea kuwa na misimamo kuwa zile ni fedha halali. Nini kinachotokea hii leo? Wanawezaje tu kuzirudisha kienyeji namna hii?

Kama kweli taifa langu lingekuwa na sheria zinazokata kotekote, Asofu Kilaini ni Askofu wangu, mimi ni Mkatoliki. Huku Marekani, wapo Wachungaji, Maaskofu, Mapasta, Mapadre wako gerezani, walishtakiwa na kufungwa, kama watu wengine. Siwezi kuwatetea watu walioshiriki kuliibia taifa, hata kama angelikuwa papa wa Kanisa!

Unamshughulikiaje Rugemarila kwa wizi wa fedha zile kama mwizi mkuu, halafu ukamuacha Jaji wa Mahakama Kuu ambaye alipokea fedha za umma kama rushwa au fedha haramu, JAJI! Jaji unamstaafisha kwa maslahi ya umma, yeye hawezi kukaa jela! Kwamba Jaji ana mke mzuri na muhimu kwake kuliko Ruge? Double Standard!

Chenge. Pamoja na kushiriki kwenye masakata yote makubwa ya wizi kuanzia Rada n.k. na bado kupokea Bilioni 1.6 za Rushwa kutoka kwa Rugemalila, Chenge ameendelea kuwa mtu muhimu ndani ya CCM na nchi, na leo hii Chenge ni Mwenyekiti wa Bunge. Kweli, are we serious? Yani Rugemalila yuko gerezani kwa makosa makubwa, lakini walionufaishwa na fedha zinazomponza Rugemalila wanapeperusha bendera za serikali mitaani?

Yani inaingiaje akilini kuwa umuweke Mdee ndani saa 120, umuweke Lema gerezani miezi minne n.k lakini Chenge yeye yuko mtaani tu! Aisee tunadanganyana sana! Hivi Chenge na Lema nani ameihasidi nchi hii to DEATH? Hivi Chenge na Mdee nani ameichafua nchi hii? Yani hawa wanaotoa maoni yao, na kushauri na kuonya serikali, wao wanaishia jela. Yale majizi makubwa yanadunda mtaani AND YET watu wanakwambia nchi imebadilika kwelikweli, JPM ameinyoosha!

Na kichekesho kikuu kinaweza kuwa kwamba, hata hao wanaochukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani, TAKUKURU haifanyi hivyo kwa weledi wao, bali wana BIP kwa Rais na kuona kama angelipenda mtu fulani afikishwe mahakamani. Sote tunajua kuwa kwa Utawala wa sasa hakuna anayefanya maamuzi, kila kitu watu wanasubiria kupima upepo ikiwa kina madhara kwao (kitamfurahisha Rais au La!) Maana kwa sasa unaweza kufanya maamuzi mazuri lakini Rais asiyapende, utatumbuliwa, na ukifanya maamuzi mabaya akayapenda unaweza kubaki (na kinyume cha kila moja), kwa hiyo pona pona yako ni kutokufanya lolote hadi uwe na uhakika kuwa litamfurahisha Rais.

Unaweza kukuta TAKUKURU wana ushahidi dhidi ya Askofu wangu Kilaini, kwamba anastahili kushtakiwa, lakini unaweza shangaa wakubwa wanawaambia, “huyo mwacheni, huyo ni Askofu!” Kwa kweli hili ndilo taifa tunalojenga, taifa linaloongozwa na utashi wa mtu mmoja mmoja katika uongozi kuliko kuongozwa na taasisi ambazo zinafuata standards (viwango).

Nchi zinazofuata standards 9viwango), Askofu akibaka, na Mvuta bangi akibaka, wote watashtakiwa na wote watafungwa ikiwa wana hatia. Lakini kwa Tanzania, Ruge na Chenge wataiba pesa na kugawana, kisha Ruge atakwenda gerezani na Chenge atabaki mtaani, na bado watanzania wanapiga makofi kuwa hatua zinachukuliwa! Tutasubiri milele, kama hakuna STANDARDS katika hatua zetu hatutapiga hatua. Kama tukisubiri kuongozwa na sauti ya mtu mmoja hatutakwenda mbele.

Tunaendelea kujenga taifa lenye ubaguzi mkuu na lenye aibu. Ndiyo maana leo Rais anakwenda Sengerema anahutubia mkutano wa chama chake kwa kigezo cha URAIS wake lakini vyama vingine vimezuiliwa kufanya mikutano, hata ya ndani, na wapo watu wanashangilia kuwa “ngoja awakomeshe wapinzani, 2020 wawe wamemalizika” na anayesema hayo ni mtanzania masikini ambaye hata bima ya afya ya uhakika hana.

Nani amesema kuwa kwa hatua hizi za DOUBLE STANDARDS za sasa eti Mbowe anakomeshwa? Eti Maalim Seif anakomeshwa? Eti Mbatia anakomeswa? Eti Zitto Kabwe anakomeshwa? Hivi hata hiyo 2020 ikiwa watanzania wataichagua CCM kwa asilimia 100, Zitto ataathirikaje? Mbatia ataathirikaje? Maalim ataathirikaje? Mbowe ataathirikaje?

Yani tu-assume kuwa wote siyo wabunge na wako mitaani tu, wataathirikaje kukushinda wewe ambaye hadi leo hujui utaajiriwa lini na nani? Au wewe ambaye umeajiriwa na mshahara wote unatumika kupandia daladala na kula lunch?

Nchi yetu inapoendeshwa kwa DOUBLE STANDARDS (Viwango viwili au zaidi kwa jambo lile lile au linalofanana na lilelile) au kwa kuchukua hatua dhidi ya watu fulani na siyo wengine kwenye jambo lilelile, nchi hiyo haiwezi kupiga hatua, itakuwa inarudi nyuma kweli kweli.

Kwenye masuala ya STANDARDS katika masuala ya msingi yanayohusu nchi na sheria zake, askofu ana wajibu uleule alionao mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Rais ana wajibu ule ule alionao mama kule kijijini Kiabakari, Mwenyekiti wa Chama cha Siasa kinachoongoza dola ana haki na wajibu ule ule wa yule Mwenyekiti wa chama ambacho hakina dola, Shehe ana wajibu ule ule ambao anao mfanyakazi au mkulima. Sote tuna wajibu katika (viwango) standards zetu.

Tukiendelea kwenda mbele bila STANDARDS tutaona baadhi ya watu wanakomeshwa na wengine wakila bata! Kwangu mimi, Rugemalila ana haki sawa sawa na Chenge, na Ngeleja, na Tibaijuka n.k. Rugemalila ni binadamu pia, ana watoto, mke ndugu n.k. na wana uchungu naye.

There is no way kwamba ASKOFU/WAZIRI/MBUNGE fulani yeye ni muhimu katika nchi kuliko na ana utaratibu tofauti mbele ya sheria na haki tofauti na mtu wa kawaida. Ndiyo maana kila siku nasema na nakumbusha maneno ya Obama alipokuwa Ghana, “Africa does not need strong men, it needs strong institutions” (Afrika haihitaji watu imara, inahitaji taasisi imara).

Mfano huu wa Obama kwa baadhi ya watu wanaofikiri kinyume chake, nawapa changamoto, wale wanaoamini kuwa JPM ni Rais bora sana, anapambana na rushwa, ufisadi n.k. NATAKA niwaambie kuwa kama huo uimara wa JPM hatautumia kujenga taasisi imara, na akaendelea kujilimbikizia madaraka na amri na kila kitu, baada ya miaka yake mitano AU kumi kuisha. Tanzania itabakia na Bunge dhaifu, Mahakama dhaifu, Serikali dhaifu, TAKUKURU dhaifu na kila kitu dhaifu. Na hapo ndipo wale watetezi wa hoja kuwa ujenzi wa taasisi imara unahitaji watu imara, wataelimika KWAMBA kiongozi imara asiyejenga taasisi imara ni sawa na mtu anayechota maji kwa kutumia tenga.

Kitendo cha kaka yangu NGELEJA nakiita cha kishujaa kwa sababu kimeivua nguo SERIKALI nzima, kwamba mwizi anaweza kusimama hadharani na kutamba kuwa anarudisha fedha za wizi na baada ya tambo zake akarejea hadi kwake na kulala huku wezi wenzie waliomuibia fedha hizo wako gerezani. Yani ni sawa na mmeibiwa NG’OMBE, mwizi halisi mkamkamata na huku mkiwajua wale ambao mwizi alikwenda kuficha ng’ombe hiyo kwao na wao wakijua ng’ombe ni ya wizi na wakakaa na ng’ombe kwa miaka kadhaa kisha siku moja wanairudisha bila hofu na mnaipokea na mnawaacha watunza ng’ombe ya wizi wakirejea makwao huku mwizi mkuu yuko gerezani!

Nakushukuru sana kaka Ngeleja, Shujaa wangu wa leo!

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.