JESHI LA POLISI LINAWASHIKILIA WATU WATATU KWA TUHUMA ZA KUMUUA MZEE WA MIAKA 60.

 

Na Allawi Kaboyo,Kagera.

Watu watatu wakiwamo mgambo wawili, wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za kumpiga na kumuua mzee mmoja aitwaye Daud Rwenyagira (60) mkazi wa kijiji Nyakahita wilayani Karagwe, baada ya kumtuhumu kuwazuia kufanya kazi yao ya kumkamata mtu aliyekula fedha za manunuzi ya kahawa.

Akizungumzia tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Kagera,Revocatus Malimi amesema kuwa mgambo hao walitumwa na mtendaji wa kijiji Nyakahita, kwenda kumkamata Theophil Pima, baada ya kulalamikiwa na mama aitwaye Mali Byamanyirwohi aliyemtuhumu kula hela zake za kununulia kahawa (BUTURA) na akawa ameitumia kwa manufaa yake binafsi.

“Baada ya mgambo hao kumkamata Theophiles Pima marehemu aliwataka wamuachie kwa kuwa ni siku ya jumapili na suala lenyewe ni la (BUTURA) yaani madai ambayo siyo sahihi kisheria” alisema kamanda Malimi.

Kamanda Malimi amesema kuwa mgambo hao walimpiga mzee huyo ngwara akaanguka chini na kuanza kumkanyaga kifuani hadi alipopoteza maisha, na kuwa mbali na kuwakamata mgambo hao pia Theophil Pima amekamatwa kwa mahojiano.

“ Watuhuiwa Jackson Bonaventura Kasenene,miaka 36 Mgambo mkazi wa nyakahita na Paul berebera Kabeibi Mnyambo miaka 26 Mgambo mkazi wa Nyakahita,shahidi muhimu Theophile Pima pia anashikiliwa kwa mahojiano zaidi”alifafanua kamanda Malimi.

Kutokana na tukio hilo,kamanda huyo anatoa rai kwa wananchi mkoani Kagera, kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, na badala yake kama wana malalamiko watumie vyombo vilivyowekwa kisheria kupata haki.

Mwezi uliopita waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akiwa ziarani mkoani Kagera, alipiga marufuku ununuzi wa kahawa usiofuata utaratibu ambao unachangia uwepo wa biashara ya magendo, hatua iliyowaondoa kazini baadhi ya watendaji wa polisi,akiwamo aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Kagera, Augustine Ollomi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.