JESHI LA MAGEREZA:TUNAWAPA UJUZI WAFUNGWA ILI WAKITOKA WAACHE UHALIFU

Inaelezwa kuwa ni muhimu wafungwa  kujifunza shughuli za Ujasiliamali wanapokuwa wanatumikia kifungo Gerezani kwakuwa zitawasaidia kujitegemea pindi watakaporejea uraiani.

Hayo yalielezwa na Mrakibu wa Jeshi la Magereza kutoka makao makuu ya Jeshi hilo Dar es Salaam  Dedan Biralo,wakati wa Maonyesho ya viwanda vidogo SIDO yanayofanyika Kitaifa viwanja vya Nyakabindi wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Akizungumza na Waandishi wa habari waliotembelea banda la maonyesho ya bidhaa za Magareza Biralo alisema kuwa moja ya kazi ya Magereza ni kutoa ujuzi kwa wafungwa ili wakitoka waache uhalifu lakini pia kuwajengea uwezo wa kutengeneza na kuzalisha bidhaa mbalimbali kupitia kazi za mikono.

” Wapo wafungwa walio na ujuzi wao lakini wapo wengine wameingia gerezani wakiwa hawana ujuzi wowote wamejifunza wakiwa ndani ya gereza,kuna wasusi wa vikapu,mikeka ,vitambaa vya kufuma kwa mkono na vya kudalizi,mafundi ujenzi na wajuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali” alisema Biralo.

Biralo alizitaja bidhaa zinazotengenezwa na wafungwa kutoka Magereza mbalimbali nchini ni pamoja na Vikapu vinavyotengenezwa Gereza la Isanga -Dodoma,Gereza la Ukonga-Dar es Salaam,Sabuni zinazotengenezwa Gereza la Ruanda-Mbeya,Viatu vya ngozi kutoka Gereza la Karanga- Moshi.

Alitaja bidhaa zingine ni Mafuta ya Alizeti kutoka Gereza la Ushora-Singida,Vitambaa vya kufuma kutoka Morogoro,Vitambaa vya kudalizi na mikeka kutoka Gereza la Ukonga,Sweta kutoka Gereza la wanawake la Kinguluila,Vikoi Gereza la Butimba- Mwanza na Mapambo Gereza la Njombe.

Biralo aliongeza kuwa Jeshi hilo linatengeneza bidhaa kutoka kwenye viwanda ambapo alisema bidhaa ya vikapu na mikeka inatengenezwa kwa nyuzi za katani ambazo zinatokana na shamba la mkonge  la Kilondo lililopo mkoani Morogoro na Mawenzi -Tanga yanayomilikiwa na Jeshi hilo.

Carren  Msangi alisema kuwa elimu ya ujasiliamali ni muhimu kwakuwa umfanya mtu kutokuwa tegemezi na kupitia ujuzi alionao utengeneza bidhaa mbalimbali na hivyo kumwingizia kipato.

Restuta Joseph mkazi wa Bariadi akinunua bidhaa za Magereza alisema bidhaa hizo zimetengenezwa kwa viwango huku akiwapongeza wafungwa kwa shughuli za kujitolea katika uzalishaji lakini pia kuhiari kupata ujuzi kutoka Katika Jeshi hilo.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.