IKUFIKIE HII KUTOKA MEZA YA MBUNGE VITI MAALUMU SUZANE MAKENE.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Mkoa wa Mwanza, Mhe. Susanne Maselle Makene, ameweka historia mkoani hapa kwa kukabidhi kiwanja chenye ukubwa wa ekari moja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Chama Mkoa wa Mwanza.


Mbunge huyo amekabidhi kiwanja hicho Jumamosi Oktoba 14, mwaka huu, kwa Uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza, akisema ilikuwa ni moja ya malengo yake kufanikisha chama kumiliki eneo lake kwa ajili ya kujenga ofisi pamoja na matumizi mengine mbalimbali.
Akikabidhi kiwanja hicho kilichoko eneo la Ndofe, Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana, Mbunge huyo ametoa wito kwa uongozi wa chama mkoani hapa kuweka mikakati kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili ujenzi wa ofisi  ya mkoa uanze mapema iwezekanavyo.

“Chama chetu kimezidi kuimarika. Lazima tujitahidi kukifanya kuwa taasisi imara zaidi kadri tunavyojipanga kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020 kufikia lengo kuu la kuchukua dola na kuongoza serikali. Hivyo ni wakati mwafaka kabisa kumiliki mali zetu kama hivi. Kiwanja hiki nimekitoa na kukikabidhi kwa uongozi wa mkoa na kitakuwa mali ya chama rasmi kuanzia leo,” alisema Mhe. Susanne.

Mhe. Susanne Maselle Makene pia amezindua jiwe la msingi lililojengwa katika mahali hapo ikiwa ni ishara ya kukabidhi na ishara ya kuwa tayari kwa ujenzi wa ofisi kubwa katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, kwa niaba ya uongozi wa Chama mkoani hapa, Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Injinia Vedastus Patrick, alimpongeza Mhe. Susanne Maselle Makene kwa uamuzi huo na namna ambavyo amekuwa akiitendea haki nafasi yake kwa kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kadri ya wajibu wake kama Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza. 

“Sisi sote ni mashahidi Mheshimiwa Mbunge wetu amekuwa akiitumikia nafasi yake ya ubunge kadri inavyotakiwa. Ndani ya hiki kipindi cha miaka miwili tu amefanya kazi nyingi ambazo zinaonekana.
 Kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Mkoa nakupongeza sana Mbunge na uendelee kwa moyo huo huo wa kujituma na kutumikia nafasi hiyo,” alisema Mzee Patrick.

Naye Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Leonard Nundi, akizungumza baada ya makabidhiano hayo yaliyofanyika kwa kusaini hati maalum ya makabidhiano, alimpongeza Mhe. Susanne Maselle Makene, kwa uamuzi huo wa kipekee ambao utasaidia kuimarisha na kurahisisha utendaji wa shughuli za chama, na kuongeza kuwa wamepokea wito wa Mbunge wa kuanza mipango ya ujenzi wa ofisi mapema iwezekanavyo.

Mhe. Mbunge anaendelea na ziara ya ujenzi wa chama katika maeneo mbalimbali ya majimbo ya Mkoa wa Mwanza aliyoianza Oktoba 13, mwaka huu kwa kutembelea vikundi mbalimbali, kuzindua matawi, kugawa vifaa vya uenezi wa Chama na kuhamasisha mkakati wa ujenzi wa chama kuanzia ngazi ya chini kupitia programu ya CHADEMA ni Msingi  ambapo baada ya kukabidhi kiwanja hicho alikutana na Kamati za Utendaji za Chama katika majimbo ya Sengerema na Nyamagana.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.