FREDDY LOWASSA ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA MONDULI

ARUSHA.

Mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa, aitwaye Freddy Edward Lowassa, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge Jimbo la Monduli mkoani Arusha, na kuwa miongoni mwa wanachama watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliochukua fomu, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga alijiuzulu na kujivua uanachama wa Chadema na kuhamia CCM.

Akizungumza na Mtandao wa Darmpya.com leo Agosti 9, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Mheshimiwa Aman Golugwa amesema Fred amechukua fomu na kurejesha.

Mbali na hivyo, Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha, aliwataja wagombea wengine, ambao ni Cecilia Ndosi ambaye ni Mwenyekiti Baraza la Wanawake wa Chadema mkoa Arusha na Diwani viti maalum, Yona Laizer, Lobulu Kivuyo na Eric Ngwijo.

Aidha, Kiongozi huyo amebainisha kuwa wagombea hao watapigiwa kura za maoni katika kikao kitakachofanyika hapo Jumamosi katika Kata ya Migungani wilaya ya Monduli.

“Kabla ya majina kufika Kamati Kuu, kuna kikao kinachoratibiwa na ofisi ya Kanda ya kanda ya kaskazini na baadaye majina yatapelekwa huko,

“Kikao kitafanyika Kata ya Migungani ambako kuna uchaguzi mdogo sasa hivi na hata hivyo imani yetu ni kwenda kutetea jimbo letu,” amesema Golugwa.

Pichani ni Freddy Lowassa akiwa na Mbunge jimbo La Mbeya Mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ‘SUGU’.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.