DRC:HUDUMA YA INTANETI NA KUTUMA SMS YAKATWA GHAFLA MPAKA MATOKEO YA UCHAGUZI YATAKAPOTANGAZWA.

Kinshasa, DRC.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekata huduma ya intaneti na ujumbe wa mfupi wa simu za mkononi (SMS) kote nchini humo kwa siku ya tatu mfululizo hii leo wakati nchi hiyo ikisubiri kwa hamu kubwa matokeo ya kwanza ya uchaguzi wa Rais.

Hali hii imetokea kuanzia juzi Desemba 31 kufuatia uchaguzi wa Rais nchini humo, uliofanyika Jumapili iliyopita, huku baadhi ya mikoa ikigubikwa na ghasia na machafuko.

Pande mbili za upinzani na muungano wa chama tawala hapo juzi (Desemba 31) zilieleza kuwa, zinaelekea kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo ambapo Wakongo wengi walishindwa kupiga kura kutokana na kuenea kwa ugonjwa wa Ebola, mapigano ya kikabila na matatizo ya mitambo ya kupigia kura.

Bw Barnabe Kikaya bin Karubi mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Joseph Kabila wa Kongo amesema kuwa huduma za SMS zilisitishwa ili kudumisha hali ya utulivu nchini baada ya kuanza kuenezwa matokeo ya uongo katika mitandao ya kijamii.

Aidha, aliongeza kuwa kuanza kusambaa kwa matokeo hayo ya uongo kunaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika machafuko na kufafanua kuwa huduma za intaneti na SMS zitaendelea kusimamishwa hadi hapo matokeo kamili ya uchaguzi yatakapotangazwa tarehe 6 mwezi huu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.