DC RUANGWA AMTUMBUA AFISA MTENDAJI ALIYESEMA HAWEZI KUPANGIWA CHA KUFANYA NA SERIKALI.

Na Bakari Chijumba, Mtwara.

Mkuu wa wilaya ya Ruangwa Mheshimiwa Hashim Mgandilwa amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,kumbadilishia majukumu ya kazi mtendaji wa kijiji cha mtimbo, Chande .N.Chande kwa kile kinachodaiwa mtendaji huyo amegoma kusimamia maendeleo kwenye serikali ya CCM kwa kuwa yeye yupo CUF.

Mgandilwa Ametoa tamko hilo kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha mtimbo kilichopo kata ya Likunja wilayani Ruangwa, 06 Disemba 2018.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo, kutokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa mtendaji huyo ni mtoro kazini na pia amedaiwa kukwamisha maendeleo ya kijiji kwa kuendekeza itikidai za vyama huku akijipambanua kuwa yeye ni CUF na hawezi kuhamasisha shughuli za maendeleo kwenye serikali ya CCM.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, mmoja wa wananchi, Bi. Ngonza Sidflide, amesema mtendaji huyo amekuwa na tabia za kuwajibu kuwa yeye hawezi kuhamasisha shughuli za kimaendeleo, kwasababu yeye ni mwanachama wa Chama cha Wananchi CUF.

“Mtendaji amekuwa na tabia ya kutokufika kazini na kusababisha wananchi tukose huduma tunazoitaji na akiulizwa anasema yeye anajipangia muda na siku ya kufika kazini na kwamba yeye ni CUF hawezi kupangiwa cha kufanya kwenye serikali ya CCM” amesema Bi.Ngonza

Aidha Bi. Ngonza ameendelea kusisitiza kuwa, mtendaji Chande amekuwa na utaratibu wa kujichagulia muda na siku za kufika kazini na huku akijitapa kuwa yeye anajipangia na hapangiwi cha kufanya.

Baada ya malalamiko hayo, mkuu wa wilaya akaagiza Hatua za kiuchunguzi zifanyike mara moja kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa mtendaji lakini wakati anasubiri uchunguzi apangiwe majukumu mengine, huku akiwataka watumishi wengine kutokuwa na tabia kama za mtendaji huyo.

“Unakuwa muajiriwa wa serikali alafu unafanya mambo ya kijinga kama ya Chande, wewe hufai kuwa muajiriwa wetu ukatafute kazi sehemu nyingine kabla sijakubaini, siwezi kumfumbia macho mtu anaekwamisha serikali” amesema Mgandilwa

Katika kuweka mkazo juu ya hilo, Mgandwila amemtaka ufisa utumishi wa wilaya kutompangia Ndg.Chande, kazi ya utendaji katika kijiji chochote kile kilichopo ndani ya Wilaya.

” Sitaki kumuona huyo katika vijiji vyangu, mtoe umpeleke hata kufagia ofisi halmashauri na si katika hivi vijiji sitaki kumuona kabisa haiwezekani amrudishe nyuma Rais wetu” amesema Mgandilwa.

Katika hatua nyingine, Mgandilwa amewataka viongozi pamoja na wananchi wa Ruangwa, kuacha kufanya siasa zisizoleta maendeleo na kuingiza itikadi za vyama kila sehemu, bali wanachotakiwa kufanya ni kushirikiana katika kutatua changamoto kwenye maeneo yao.

“Mpaka sasa nimetembea katika vijiji 70, vijiji hivi vyote vinachangamoto za barabara, vyumba vya madarasa, zahanati, nyumba za wauguzi na walimu, hatuwezi kutatua changamoto hizi kama tutakuwa na viongozi ambao si sahihi”

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.