DC MJEMA AAGIZA TAKUKURU KUWACHUKULIA HATUA WAFANYABIASHARA WANAOUZA MAENEO NA VIZIMBA

Dar es Salaam

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema amemuagiza Afisa wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ilala kufanya uchunguzi kwa wafanyabiashara wanaouza maeneo ya biashara katika Kata ya Kariakoo na vipande vya barabara.

Mjema ameyasema hayo leo, katika Kata ya Kariakoo wakati akifunga ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua katika majimbo ya yaliopo wilayani humo, ikiwemo Ukonga, Segerea pamoja na Ilala.

Amesema kuwa, katika kata hiyo kero kubwa aliyokutana nayo ni wafanyabiashara hao kutoshirikishwa katika ngazi ya maamuzi ambapo hadi n sasa wameshasikiliza kwa asilimia 85 ambapo kwa asilimia 65 wameshatolea uamuzi na zilizobaki wamezichukua kwa ajili ya kujishughulisha.

“Mpaka sasa nimeshaskiliza kero kwa asilimia 85 katika majimbo yote niliyoyatembelea ambapo nimeshazitolea uamuzi kwa asilimia 65 zilizobaki nimezichukua kwa sababu ni za taasisi mbalimbali ikiwemo,Takukuru, Bima ya afya, Tarula,Tanesco pamoja na Dawasa “amesema DC Mjema

“Nakuagiza Afisa Takukuru Ilala kuanzia kesho anza uchunguzi kwa wafanyabiabiashara wanaouza vipande vya barabara, na wale wanaowapangisha wenzao na kupokea pesa”amesema Mjema.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya mfanyabiashara mmoja kutoa kero kwa mkuu wa Wilaya huyo, kuwa amekamilisha tararibu zote za kupata meza lakini mpka sasa hajapata meza jambo ambalo limekuwa kikwazo sokoni hapo.

Aidha amemuagiza Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala, kuanza upya kupanga tena meza hizo kutokana na kukosekana utaratibu mzuri wa kufuata kwa wafanyabiashara hao kuonekana mtu mmoja anamiliki meza tatu hadi sita.

“Nakuagiza Afisa Biashara Ilala naomba uanze upya kupanga meza hizi kwani hapa inaonekana wameshindwa kujisimamia wenyewe wanapangishana mpaka vipande vya barabara hili jambo ajabu sana hivyo, hili zoezi lianze upya ” amesema DC Mjema.

Amesema kuwa, zoezi hilo la kugawa upya meza za wamachinga Kariakoo litaanza Octobar 26 mwaka huu ambapo amemwagiza Afisa Masoko kuanza taratibu wa kupanga kwa kushirikiana na Afisa Biashara.

Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala amezindua miradi ya Maendeleo na kufanya utatuzi wa kero za wananchi ambapo DC huyo ameongozana na wataalam mbalimbali na pamoja na wakuu wa Idara kwa ajili ya kutatua kero za wananchi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.