DC KILOLO ASIA ABDALLAH ATATUA MGOGORO WA UJENZI WA SEKONDARI YA KATA

Na  Francis Godwin Dar Mpya  Iringa

MKUU  wa  wilaya ya  Kilolo  mkoani Iringa Asia Abdallah  amemaliza mgogoro  uliodumu kwa  miezi  zaidi ya  minne  juu ya eneo la  ujenzi wa shule ya  sekondari ya kata ya Mahenge  baada ya  kijiji  cha Mahenge  kugoma  kuungana na vijiji viwili  vya  Maganga na Irindi kujenga sekondari  moja  ya kata  na   kutaka  kujenga sekondari yake  ya  Kijiji  cha Mahenge pekee.
Pamoja na  kumaliza kutatua  mgogoro  huo  mkuu  huyo wa  wilaya  ya  Kilolo  ametoa onyo kali kwa  viongozi  wanaotumia vikundi  vya  watu  kumchafua Rais Dkt  John Magufuli ama  kukwamisha  jitihada  mbali mbali  za  serikali  kwa  kuwataka  viongozi  hao  kujitathimini  upya  kabla ya  kuchukuliwa  hatua za  kimaadili .
Mkuu huyo  wa wilaya ambae  aliongozana na kamati yake ya  ulinzi na usalama na  viongozi wa  vijiji  vinavyovutana  pamoja na wataalam kutoka  ofisi ya  Halmashauri  walifikia  makubaliano  hayo  jana  katika  mikutano  ya  hadhara  iliyofanyika  katika   vijiji vyote vitatu  vya Magana ,Irindi na  Mahenge  pamoja na  kukagua eneo  lililotengwa kwa  ajili ya  ujenzi wa  sekondari ya kata  inayoungwa mkono na wataalam  na  vijijini  vya Magana na  Iringa  pia  kutembelea  eneo  lisiloungwa mkono  na  vijiji  viwili la Mahenge ambalo  kijiji cha Mahenge  wanataka kujenga  sekondari .
Akizungumza na wananchi wa vijiji  vya kata ya Mahenge katika mikutano ya  hadhara  mkuu  huyo wa  wilaya ya  Kilolo  alisema  kuwa serikali imeagiza  ujenzi wa  sekondari za kata kwa  kila kata  lengo  likiwa ni kuepusha  watoto  kusafiri  mwendo  mrefu  kupata elimu  na kuwa  serikali haiingilii  wananchi  wapi  shule  ya sekondari inapaswa  kujengwa bali  wananchi  wanaamua na  serikali inatuma  wataalam  wake  kukagua  eneo  husika .
“Vikao  vya maendeleo ya  kata  ndivyo ambavyo vinaamua  wapi  shule  ijengwe  na  katika kata  hii  nimeelezwa  kuwa  kikao  cha  kata  kilikaa na  kuamua  shule  kujengwa kijiji cha Irindi  ambacho  kipo katikati ya Magana , Irindi na  Mahenge  na wataalam  walifika  kukagua na  kubariki eneo hili  kuwa   ni sahihi kwa  ujenzi wa sekondari  lakini kijiji cha Mahenge  viongozi  wake  wamegeuka maamuzi na  kwenda  kuanza  kuandaa kiwanja  kwa  ajili ya shule yao ya  kijiji   hili  haliwezekani ”  alisema  mkuu  huyo wa wilaya  ya  kilolo
Kuwa  kilichofanywa na  uongozi wa  kijiji cha Mahenge  ni kinyume na utaratibu  pia  wamekata  miti  na kuharibu mazingira kinyume na sheria  za  mazingira  jambo ambalo hakuna kiongozi  wa  serikali atalifumbia macho .
Alisema  kama  viongozi  wote  walikubaliana  shule  kujengwa  kijiji cha Irindi ambako ni katikati  hakukuwa na  sababu ya  viongozi wa  kijiji cha Mahenge  kufyeka  miti na  kuandaa eneo la  ujenzi wa sekondari ya  kijiji  ambayo  kwa mujibu wa  serikali ya  elimu na mipango ya  serikali  bado hatua ya  ujenzi  wa  sekondari ya  kijiji  haijafika  kwa  sasa ni  kila kata  kuwa na sekondari  yake na sio  kila kijiji na iwapo kijiji cha Mahenge  wataona  ina faa  basi eneo hilo  kuliandaa kwa  ajili ya  ujenzi wa  kituo  cha michezo ama  kidato cha tano na  sita  ila  baada ya  kumaliza  ujenzi wa  shule ya kata  uliopangwa  kushirikisha  vijiji  vyote vitatu .
Hata  hivyo  mkuu  huyo wa wilaya  alisema  hajapendezwa na  baadhi ya  viongozi wa kijiji cha Mahenge  kuunda  vikundi vya  vijana kwa  ajili ya kukwamisha  jitihada  mbali mbali za  serikali ya  awamu ya  tano  pamoja na kufanya  uchochezi wa  wananchi  kuichukia  serikali kuwa  jambo  hilo  halitavumiliwa na  kuwataka  kuacha mara  moja .
Kufuatia  mikutano  hiyo viongozi wa  kijiji cha Mahenge  na  wananchi  walikubali kuungana  kujenga  sekondari ya pamoja katika  kijiji cha Irindi kama  ilivyopangwa na  kuomba  msamaha  kwa  mkuu  wa wilaya kwa  wote  yaliyojitokeza  kwani   walilazimika  kuanza  ujenzi wa  shule yao ya  kijiji kwa nia njema ya  kuwasaidia  watoto  wao  wasome  jirani lanini  walifanya  hivyo  baada ya  kuhamasishwa na  aliyekuwa katibu  tawala wa mkoa wa Iringa  Wamoja  Ayubu .
Katika  hatua  nyingine  mkuu wa  wilaya ya  Kilolo amepiga marufuku  viongozi wa vijiji  vinavyounganisha kata ya  Mahenge  kuwalazimisha wananchi kutoa  michango ya  ujenzi  wa  sekondari  hiyo na badala yake ameshauri  wananchi  kuelimisha  ili  kujitolea  pasipo  kunyanyasana  kwani  alisema  Rais Dkt Magufuli  hataki  wananchi  wanyanyasike  katika  kushiriki  shughuli za kimaendeleo .

Mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Asia Abdallah akizungumza na wananchi wa kijiji cha Irindi katika mkutano wake wa kutatua mgogoro wa ujenzi wa sekondari ya kata ya Mahenge

Wananchi wa kijiji cha Irindi kata ya Mahenge wilaya ya Kilolo wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah (hayupo pichani ) wakati wa mkutano wa kutatua mgogoro wa ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Mahenge
Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah wa kwanza kushoto akitazama miundo mbinu ya maji iliyosogezwa eneo la ujenzi wa sekondari ya kata ya Mahenge kijiji cha Irindi jana
Wajumbe wa kamati ya ulini na usalama wilaya ya Kilolo na wataalam wa Halmashauri wakiwa na mkuu wa wilaya ya Kilolo kukagua eneo la ujenzi wa sekondari ya kata ya Mahenge kijiji cha Irindi jana
Viongozi wa kijiji cha Mahenge wakiwa katika eneo ambalo wamekata miti kutaka kujenga sekondari yao ya kijiji wakipinga ujenzi wa shule ya kata nje ya kijiji chao jana
Wananchi wa kijiji cha Mahenge wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wakiwa katika mkutano wa hadhara na mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah jana
Mmoja kati ya wananchi wa kijiji cha Mahenge akitoa maoni yake katika mkutano wa mkuu wa wilaya ya Kilolo juu ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Mahenge

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.