CUF YAMPA MAKAVU JULIUS MTATIRO NA JINSI ALIVYOTAKA KUISAMBARATISHA CUF

Na mwandishi wetu

 

Chama cha Wananchi (CUF) kimemtolea uvivu na kumpa makavu yake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho Julius Mtatiro kwa kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja zake alizozitaja kwenye mazungumzo yake aliyofanya na wanahabari Unguja.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa wanahabari na Abdul Kambaya, Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mahusiano na Umma CUF, chama hicho kimesema Mtatiro anatafuta njia ya kupata uongozi wa serikali chini ya CCM kwani ndiyo hoja yake ya msingi aliyoitoa wakati anakihama chama hicho, hivyo kuongea hoja zake zisizo na msingi na kuuponda upinzani ni njaa ya madaraka.

Kuhusu ufafanuzi wa hoja zake CUF imesema yeye kuitwa kafiri kipindi yupo CUF ni hoja dhaifu kwa kuwa alipaswa kulieleza hilo kipindi kile kile alipokua ndani ya chama ili hoja yake iwe na mashiko.

“Vikao vya Chama ndivyo venye uwezo wa kushughulikia masuala ya nidhamu ya wanachama na si vinginevyo na kwa bahati nzuri kipindi hicho anachokisema, yeye Mtatiro alikua ndie Naibu Katibu Mkuu Bara kwa hivyo hakua na tatizo la kuandaa na kuitisha kikao kwa mujibu wa katiba ya chama ili kushughulikia tatizo tajwa kwenye ufafanuzi wa hoja zake” – Abdul Kambaya.

Aidha chama kimemtupia lawama Mtatiro kuwa yeye ndiye aliyekivuruga chama na wala si Lipumba, yeye ndiye aliekua mwenyekiti wa mkutano mkuu maalum uliojadili pamoja na mambo mengine lakini pia ulijadili barua ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba nafasi ya mwenyekiti taifa.

“Mtatiro kwa kutii maelekezo ya Maalim Seif alikiuka katiba ya CUF katika kuendesha mkutano ule na kupelekea kuvunjika, Mtatiro ndyie aliekua anamshauri vibaya Katibu Mkuu na ndiye aliechangia kutufikisha hapa tulipofika. Kwenye mgogoro wa CUF Prof Lipumba hoja zake zipo wazi katika chama, Prof alihitaji chama kiongozwe kwa mujibu wa makubaliano ya vikao na sio utashi wa mtu mmoja jambo ambalo yeye Mtatiro alimpinga Lipumba kwa kutegemea kuwa atapoondoka Lipumba yeye ndiye ataepewa nafasi hiyo” – Abdul Kambaya.

Pia chama hicho kimesema madai ya Mtatiro kusema CUF sio taasisi imara ni hoja dhaifu maana chama hicho kipo kikatiba na yeye na wenzake wanapojaribu kukirudisha nyuma bado kimezidi kusimama imara.

“Wanachama wamekua imara kupinga ukiukwaji wa katiba ya chama na hatimae kina Mtatiro kujikuta wamekimbilia mahakamani kufungua kesi mbalimbali za kikatiba mfano, Mtatiro mwenyewe kujiita kuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi cheo ambacho hakipo kwenye katiba ya CUF huku wapambe wake pamoja na Maalim Seif wakibariki ukiukwaji huo wa katiba. Kama CUF isingekua taasisi na isingekua imara basi ukiukwaji huo ungekubaliwa kama ambavyo yeye Mtatiro anaukubali mpaka leo, Mtatiro wakati anajiunga na CCM alisema kuwa anatoka CUF akiwa na cheo cha mwenyekiti wa kamati ya uongozi cheo ambacho hakipo kwenye katiba na Mtatiro anafahamu kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama hakuna cheo hicho” – Amesema Kambanya.

Katika hatua nyingine CUF imeshangazwa na Mtatiro kuuponda UKAWA wakati yeye ndiye miongoni mwa waliounda UKAWA na kuiwakilisha CUF kama Think Tank lakini leo hii anasema haifai.

“Leo Mtatiro anasahau na kuanza kuuponda UKAWA ambao yeye ndiye miongoni mwa Think Tank ya UKAWA? Kisha mtu huyu anajilinganisha na Prof Lipumba kwa uwezo wa kufikiri na kuona mbali katika matukio ya kisiasa? Prof ameona tatizo la UKAWA tangu mwaka 2015, Mtatiro anaona tatizo la UKAWA 2018 yaani kilichoonwa na Prof Lipumba 2015 Mtatiro anakiona miaka mitatu baadae? Kwa tofauti hii ya maono Mtatiro hawezi kulingana na Prof Lipumba kwa namna yoyote ile” Ameongeza Kambaya.

Amemalizia kwa kujibu suala la Maalim Seif kuwa zaidi ya CUF kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wale aliowaita wafuasi wa Lipumba ni kinyume cha Katiba ndio maana pengine Maalim alishindwa kufanya hivyo kwa kuwa Mtatiro hakuwa na hoja za msingi dhidi ya wale aliowaita wafuasi wa Lipumba. Hivi unamshauri Maalim Seif awafukuze watu kwa kuwa tu wanaunga mkono hoja za Lipumba kuhusu UKAWA?.

“Busara ni kufahamu kitu cha kuandika au kuongea lakini hekima ni kufahamu wakati wa kuandika au kuongea. Ni Mtatiro huyu huyu alikosoa bajeti ya 2018/2019 kwa nguvu kubwa zilizojaa mbwembwe za kila aina mpaka kusema maneno yasiyo hata na nidhamu kwa rais wa nchi lakini mwezi mmoja na nusu akasahau yote na akaamua kuunga mkono jitihada za Rais katika kusimamia maendeleo ya nchi yetu. Hapa utagundua kwamba kikichopo ndani ya nafsi yake ni mbio za kutafuta ajira na si kuunga mkono jitihada za Rais. Ni kweli wapinzani moja ya wajibu wetu ni kukosoa, lakini ukosoaji wetu unajenga umoja? Una heshima na utu wa mtu? Au unalenga kutafuta umaarufu na kujipandisha thamani ili wanunuzi wafike bei ?” – Amehoji Kambaya.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.