CIA KUZINDUA MASHAMBULIZI YA NDEGE ZISIZO NA RUBANI DHIDI YA WANAJIHAD LIBYA.

Niamey, NIGER.

Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), linatarajia kuzindua mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu wa Al-Qaeda na kundi la Islamic State nchini Libya.

Mashambulizi hayo yatatekelezwa kutoka kambi mpya ya kijeshi kaskazini mashariki mwa Niger, gazeti la New York Times limearifu leo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo la kila siku la Marekani likinukuu maafisa wa Nigeria na Marekani, operesheni za upelelezi zilifanyika kwa miezi kadhaa kutoka uwanja wa ndege mdogo wa Dirkou, ambapo usalama umeimarishwa tangu mwezi Februari mwaka huu.

Akihojiwa na gazeti la New York Times, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger, Mohamed Bazoum, alikiri kuwepo kwa ndege za Marekani zisizokuwa na rubani katika mji huo mdogo wa jangwani, bila kutoa maelezo zaidi, wakati Meya wa Dirkou, Bw Boubacar Jerome, akisema ndege hizo zimepelekea usalama kuimarika zaidi katika mji wake.

“Matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani na CIA yalipunguzwa na rais wa zamani wa Marekani Barack Obama kufuatia mashambulizi yaliyosababisha vifo vya raia wa kawaida.

“Obama alipendelea operesheni hizo kuendeshwa na jeshi badala ya shirika hilo la Ujasusi kwa udhibiti bora,” New York Times limeongeza.

Aidha, mrithi wake, Rais Donad Trump, amezindua tena operesheni za CIA kwakutumia ndege zisizokuwa na rubani kutekeleza mashambulizi, kulingana na chanzo hicho.

Pentagon ina kambi ya kijeshi huko Niamey, mji mkuu wa Niger, kilomita 1,300 kutoka Dirkou. Jeshi la Marekani limekuwa huko kwa ajili ya kuendesha mashambulizi ya anga dhidi ya makundi ya wanamgambo wa Kiislamu nchini Libya.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.