CHADEMA YALAANI VIKALI KUKAMATWA WAANDISHI WA CPJ, WATOA TAMKO KWA SERIKALI.

 

Chama Cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani vikali kukamatwa na kushikiliwa hati za kusafiri za wanaharakati wa Kamati Maalum ya Kuwalinda Wanahabari duniani, (CPJ) waliotembelea Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje CHADEMA, Ndg. John Mrema amesema kama chama wameshangazwa na sababu za kuwakamata wanaharakati hao zinazotolewa na idara ya Uhamiaji hapa nchini ya kwamba hati zao nchini zilikuwa kwa ajili ya matembezi na si kwa ajili ya kukutana na waandishi wa habari.

“Sisi kama chama tunajiuliza ni sheria ipi imewakataza watalii wanaokuja kutembea nchini kukutana na waandishi wa habari, ni sheria ipi imewakataza kukutana na viongozi wa vyama vya siasa, mbona wengine wako huko mbugani wanatembea na waandishi wa habari lakini hawakamatwi kwanini hawa wawili?” amehoji Mrema.

Aidha Mrema amesema endapo serikali itashindwa kuchukua hatua kwa haraka kwa haya yanayoendelea kutokea hapa nchini uchumi wan chi utazidi kuyumba na utalii utakufa kabisa kutokana na matukio ya uvunjifu wa sheria yanayoendelea hapa nchini likiwemo ya kukamatwa kwa wanaharakati hao.

“Serikali yetu isipokuwa makini kwenye mambo haya yanayoendelea na matukio haya basi uchumi utaendelea kuyumba, utalii utakufa nchi hii wasipokuwa makini na hatua hizi wanazochukuwa ambazo hazifuati sheria, taratibu wala kanuni” amesema Mrema.

Pia chama hicho kimeitaka serikali kuheshimu mikataba ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa maoni na uhuru wa habari na kuwatengenezea mazingira mazuri waandishi wa habari wa ndani na nje kwani ni wajibu wao waandishi kuuharisha umma.

“Tunaitaka serikali kuheshimu mikataba ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kutoa maoni na kupata habari na kuwajengea mazingira mazuri waandishi wa habari wa ndani na nje ili waweze kuuhabarisha umma” amesema Mrema.

Taarifa za awali hapo jana usiku zilisambaa mtandaoni juu ya kukamatwa kwa wanaharakati wa CPJ waliotembelea nchini Angela Quintal na Muthoki Mumo kabla ya kuachiwa huru leo na Idara ya Uhamiaji kwa masharti maalum ya kutofanya vikao na waandishi wa habari.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.