DUH!! TUME YA UCHAGUZI DRC YAAHIRISHA TENA UCHAGUZI

Kinshasa, DRC.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (CENI) hapo jana iliahirisha uchaguzi katika miji mitatu nchini humo, uchaguzi wa rais na wa bunge uliopangwa kufanyika Jumapili ya tarehe 30 mwezi huu hadi mwezi ujao wa Machi.

Hatua hii inamaanisha kuwa kura za miji hiyo mitatu hazitajumuishwa katika mchuano wa kiti cha urais.

Miji hiyo mitatu huko Congo ambayo uchaguzi umeahirishwa ni Beni na Butembo inayopatikana mashariki mwa nchi hiyo ambayo imekuwa ikisumbuliwa na homa ya Ebola tangu mwezi Agosti.

Aidha, mji wa Yumbi magharibi mwa nchi ambako watu zaidi ya 100 waliuawa wiki iliyopita katika machafuko ya kikabila nao umeahirishwa kufanyika zoezi la upigaji kura siku hiyo.

CENI pia imeongeza kuwa chaguzi hizo mbili zitafanyika kama ilivyopangwa siku ya Jumapili, na matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa rais yatatangazwa Januari 15 mwaka 2019 na Rais mpya ataapishwa Januari 18.

Itakumbukwa kuwa uchaguzi wa rais na bunge ulipangwa kufanyika tarehe 23 Disemba, ambapo siku moja kabla kuwadia Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi iliuahirisha kutokana na mkasa wa moto uliotokea ambao uliteketeza vifaa vya uchaguzi kwa ajli ya mji mkuu Kinshasa.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.