CCM WILAYA YA ILALA YAPIGA MARUFUKU WATANGAZA NIA NAFASI ZA UDIWANI

Na Heri Shaban, Dar es salaam.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ilala, kimewapiga marufuku watangaza nia katika nafasi za udiwani kata ya Tabata, badala yake wametakiwa kujenga chama.

Hayo yamesemwa jana Desemba 05, 2018 na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilala, Ndg Ubaya Chuma, wakati wa kikao cha mkutano mkuu wa chama (CCM) hicho, Tabata Mtambani jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenezi wa chama hicho ngazi ya taifa Ndugu Humphrey Polepole.

“Napiga marufuku waliotangaza nia katika nafasi za udiwani kata ya Tabata, waache tutawachukulia hatua, badala yake nawaomba mshirikiane kuhakikisha CCM inashika dola katika chaguzi zake za serikali za mitaa mwaka 2019.” alisema Ubaya chuma

Aidha, ndg Chuma aliongeza kusema kuwa, kumekuwepo na wagombea mbalimbali wameshaanza kupita (mitaani), kabla wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2020 ndani ya kata hiyo, na wote (hao wanaofanya kampeni kwa siri) watashughulikiwa.

Mbali na hivyo, kiongpzi huyo wa chama tawala ngazi ya mtaa (Tabata), amewataka (wanachama na viongozi) washirikiane ndani ya chama kwani kazi ya kiongozi ni kuhakikisha CCM wilaya ya Ilala inashika dola katika uchaguzi zote, kuanzia ngazi ya udiwani hadi Rais.

Kwa upande mwingine, Ubaya Chuma alipiga marufuku kutumia rushwa katika uchaguzi wa serikali za mtaa ambao unatarajia kufanyika mwaka 2019 ambapo wagombea wote watakao tumia rushwa majina yao yatakatwa.

Hata hivyo, ndg Ubaya akifafanua suala hilo la uchaguzi wa ndani na serikali za mitaa, alisema uchaguzi wa serikali za mitaa umeshafika utafanyika miezi ya mwanzoni mwaka 2019, hivyo CCM wilaya ya Ilala itarudisha majina matatu katika uchaguzi huo, ambayo yatapelekwa katika makao makuu ili yaweze kupigiwa kura na wanachama kwa kufuata demokrasia.

Pia mwenyekiti (wilaya Ilala) huyo aliwambia wanaCCM wa Tabata Mtambani, kuwa watambue cheo ni dhamana na kila mtu atumie cheo kwa kuendeleza mazuri ya chama sio kinyume na kanuni za chama.

Kwa upande wake katibu wa CCM Tabata Mtambani, ndg Ramadhani Kudunale, alisema CCM mtaa wa Mtambani ina wanachama Hai 586 kati yake wanawake 366 wanaume 220 na idadi ya mashina yaliopo kwenye mtaa huo ni 13.

Katibu Kudunale alielezea mafanikio katika tawi hilo, ambapo alisema viongozi wa Jumuiya wameweza kushirikiana na mabalozi wa shina kuongeza idadi ya wanachama, kufanya vikao kwa kufuata kanuni, kuongeza wanachama, pamoja kuhakikisha vikao vya kanuni vinafanyika kwa wakati.

Akizungumzia hali ya kisiasa katika eneo la Mtambani (Tabata), alisema wastani wananchi na wanachama bado wana imani kubwa na CCM kutokana na kudumishwa kwa amani, upendo na utilivu kwa nchi yetu sambamba na utekelezaji wa Ilani ya chama unaofanywa na Rais John Pombe Magufuli na viongozi mbalimbali.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.