BITEKO AKERWA NA AJALI MAENEO YA WACHIMBAJI WA MADINI MKOANI MARA.

 

Na. Augustine Richard.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Mashaka Biteko leo Januari 4, 2019 amewataka wachimbaji wadogo katika eneo la uchimbaji mji wa Buhemba wilayani Butiama mkoani Mara kuzingatia uchimbaji salama ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara katika maeneo ya migodi.

Biteko ameyasema hayo wakati wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo yaliyofanyika wilayani Butiama mkoani Mara yenye lengo la kuwafundisha wachimbaji wadogo masuala ya uchimbaji salama, uchenjuaji, afya,umhimu wa kulipa kodi na tozo mbalimbali na mazingira ya uchimbaji katika mkoa wa Mara.

“Akifa mtanzania mmoja huyo Mtanzania ni muhimu kuliko mgodi wote, kuliko mtanzania mmoja afe ni bora huo mgodi usiwepo.Buhemba ni eneo linaloongoza kwa ajali kwenye migodi, huu mgodi ulifungwa na toka umefunguliwa kuna vifo vya wachimbaji kumi na mbili na majeruhi 20″alisema Biteko

“Serikali haiwezi ikakubali hali hii iendelee nitakuja kuufunga tena mgodi huu kama hali hiyo itaendelea hatuwezi kupoteza maisha ya watanzania.Serikali haiko tayari kuona kuwa watu wanaendelea kufa ndio maana imeamua kufika na kuandaa mafunzo kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kufundishwa namna bora za uchimbaji salama na wenye tija” Naibu Waziri Doto Biteko alisisitiza.

Akihitimisha mafunzo hayo Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Butiama mkoani Mara Bi Anarose Nyamubi kwa kazi na ushirikiano mzuri baina yake na serikali pamoja na kuwapongeza wananchi wa wilayani Butiama kwa mwitikio na usikifu mkubwa katika kuhakikisha shughuli za Serikali zinafanyika kwa ufanisi wa hali juu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.