BARAZA LA MAULAMAA LA INDONESIA LATOA WITO WA KUFUKUZWA BALOZI WA SAUDIA.

 

Jakarta, INDONESIA.

Baraza hilo ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya Kiislamu nchini Indonesia limemtuhumu Osama bin Muhammad al Shuaib, balozi wa Saudi Arabia nchini humo kuwa anaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuitaka serikali ya Jakarta imfukuze haraka balozi huyo au iandae mazingira ya kuitwa nyumbani na utawala wa Aal Saud.

Inaonekana kuwa wito wa Baraza la Maulamaa la Indonesia la kutaka kufukuzwa nchini humo Balozi wa Saudi Arabia lina uhusiano kwa njia moja au nyingine na mienendo mibaya ya utawala wa Saudi Arabia na waajiri wa nchi hiyo dhidi ya raia wa Indonesia wanaofanya kazi nchini Saudia.

Ripoti mbalimbali kuhusu kukatwa vichwa na kuuliwa baadhi ya raia wa Indonesia wanaofanya kazi Saudi Arabia zimewakasirisha wananchi wa Indonesia na kuzusha malalamiko makubwa nchini humo dhidi ya watawala wa Aal Saud.

Japokuwa Rais wa Indonesia, Joko Widodo, naye amepinga pia vikali jinai hizo za utawala wa Aal Saud na kuzilaani, lakini Baraza la Maulamaa la Indonesia linaona kuwa, msimamo na hatua hiyo haitoshi na wanasena serikali ya Jakarta inapasa kulinda roho na hadhi ya raia wa nchi hiyo nje ya nchi kwa kuchukua hatua ya kumfukuza balozi wa Saudia mjini Jakarta.

Kwa upande wake Bw Sayyid Ali Wasef mchambuzi wa masuala ya Kiislamu amesema, hatua za Saudi Arabia za kuwauwa Waislamu ni jinai dhidi ya binadamu na hakuna shaka yoyote kuhusu suala hilo.

Hivyo basi, natukio yaliyojiri wakati wa ibada ya Hija na kuuliwa Waislamu huko Yemen ni sehemu ndogo tu ya jinai za Saudi Arabia dhidi ya ubinadamu.

Baraza la Maulamaa la Indonesia limekuwa likipinga vikali mitazamo na fikra za makundi ya kigaidi likiwemo kundi la Daesh (ISIS), na yale ya Kisalafi na linasisitiza udharura wa kuwepo ushirikiano baina ya wafuasi wa dini mbalimbali na kuishi pamoja kwa amani baina ya madhehebu tofauti za Kiislamu.

Mtazamo huu unapingana kikamilifu na fikra za kuweka mipaka na imani potofu za Kiwahabi ambazo watawala wa Saudi Arabia wanazieneza na kuzinga mkono kwa kutoa misaada ya kifedha kwa makundi mbalimbali.

Baraza la Maulamaa la Indonesia linaushawishi mkubwa miongoni mwa wananchi kutokana na kujishughulisha na kazi za kujitolea kama kutoa misaada mashuleni na mahospitalini na pia kuyasaidia makundi mbalimbali yasiyojiweza ili kupunguza umaskini sambamba na kujihusisha na masuala ya kidini.

Kwa msingi huo, serikali ya Jakarta inahitaji uungaji mkono wa taasisi hiyo ya wanazuoni wa Kiislamu ili kuimarisha amani na utulivu nchini na kuweza kutekeleza vyema majukumu yake.

Kwa sababu hiyo wito wa baraza hilo kwa serikali likitaka kufukuzwa balozi wa Saudi Arabia mjini Jakarta, unaakisi wasiwasi mkubwa wa maulamaa wa Indonesia kuhusu shughuli na harakati za Kiwahabi zinazofanywa na ubalozi wa Saudia nchini humo.

Aidha, Bw Chris Chiplin, ambaye naye ni mchambuzi wa masuala ya kusini mashariki mwa Asia katika Taasisi ya Utafiti ya Uholanzi amesema Saudia ilitaka kujipenyeza kupitia masuala ya kidini.

“Katika miaka kadhaa ya karibuni Saudi Arabia ilifanya jitihada za kutaka kujipenyeza na kuwa na ushawishi katika utamaduni na masuala ya kidini nchini Indonesia kupitia njia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali.

“Saudi inatekeleza hatua hizo kwa malengo maalumu kwa sababu Wasaudia wanaamini kwamba, nchini Indonesia kuna fursa na uwanja mzuri wa kuweza kuenezaji haraka fikra za kidini na kiutamaduni za Saudia; jambo ambalo linamewatia wasiwasi maulamaa wa nchi hiyo.” Amesema Chiplin.

“Alaa kul haal, jinai zinazofanywa na Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia huko Yemen, Syria na Iraq na ugaidi wa kiserikali unaofanywa na nchi hiyo kwa kuwauwa wapinzani wake yote hayo yamewakarisha sana Waislamu kote duniani wakiwemo wa Indonesia.” Amesema Chiplin.

Vilevile, katika tukio hili tunaweza kuutaja wito wa Baraza la Maulamaa la Indonesia wa kufukuzwa nchini humo balozi wa Saudi Arabia haraka iwezekanavyo kuwa ni ishara ya kukasirishwa na kutorishwa pakubwa wananchi wa nchi hiyo na mienendo ya watawala wa ukoo wa Aal Saud.

Wakati huo huo kwa kuzingatia kuwa Baraza la Maulamaa la Indonesia ndilo linabuni mipango ya kidini nchini humo, wananchi wa Indonesia pia wanataraji kuwa, baraza hilo litachukua msimamo imara dhidi ya utawala wa Saudi Arabia katika ngazi ya juu ya kidini.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.