BAADA TRUMP KUTUA KINYEMELA IRAQ, UBALOZI WA MAREKANI WASHAMBULIWA

Baghdad, IRAQ.

Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad nchini Iraq umeshambuliwa kwa maroketi mapema leo Alhamisi masaa machache baada ya Rais Donald Trump kufanya safari ya kinyemela nchini Iraq akiandamana na mkewe.

Vyombo vya habari na wafanyakazi katika eneo la al Khadhraa lenye ulinzi mkali katikati mwa Baghdad wanasema kuwa ubalozi wa Marekani mjini humo umeshambuliwa kwa maroketi mawili alfajiri ya leo.

Duru hizo zinasema alfajiri ya leo kulisikika ving’ora vya tahadhari kutoka kwenye jengo la ubalozi wa Marekani baada ya shambulizi hilo ambalo bado hasara zake hazijajulikana.

Shambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Baghadad limefanyika masaa kadhaa tu baada ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kutembelea ghafla majeshi ya Marekani huko Iraq kwa mnasaba wa sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya ujao.

Ndege ya Trump ilitua katika kambi ya kituo cha anga cha Ain al-Asad huko magharibi mwa mji wa Baghdad baada ya safari ya masaa kadhaa nyakati za usiku kutoka Washington.

Katika safari yake hiyo ya masaa matatu, Rais wa Marekani hakukutana na kiongozi yeyote wa Iraq.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul-Mahdi imetangaza kuwa mazungumzo ambayo yaliyokuwa yafanyike kati ya kiongozi huyo na Trump yamefutwa kwa sababu ya kutofautiana kuhusu namna ya kufanyika kwake.

Wabunge wa Iraq wamevieleza vyombo vya habari kuwa Trump alitaka mazungumzo hayo yakafanyike kwenye kituo cha anga cha Ain al-Asad, wazo ambalo lilipingwa na Abdul Mahdi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.