AUMUUA KIKATILI HAWALA YAKE KISHA NA YEYE KUJIUA

Na Allawi Kaboyo Bukoba.

Watu wawili wanaodaiwa walikuwa katika mahusiano ya kimapenzi wamefariki baada mmoja kunyongwa na mwingine kujinyonga, katika mtaa wa Mafumbo katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi alisema kuwa mauaji hayo yamegundulika Desemba 17 mwaka huu saa 11 jioni katika mtaa huo.

Malimi alimtaja anayedaiwa kunyongwa na mpenzi wake kuwa ni Regina Temu (29) mkazi wa Kahororo pia katika manispaa hiyo, na mfanyakazi wa kiwanda cha kusindika kahawa cha Tanica, aliyekutwa amenyongwa kwa tai.

Alisema kuwa baada ya huyo mpenzi wake aitwaye Karoli Domisian  (36) mwalimu wa  shule ya sekondari Nyanshenye iliyoko katika manispaa ya Bukoba kutekeleza mauaji hayo, naye alijinyonga palepale kwa kutumia kamba ya manila ndani ya chumba chake.

“Ndani ya chumba chake kulikutwa karatasi yenye ujumbe wa maandishi iliyoonekana kuandikwa na mwanaume, kwamba amejinyonga mwenyewe baada ya kumuua mpenzi wake, kutokana na kumsaliti” alisema kamanda huyo.

Malimi alisema kuwa Regina alikuwa akiishi na dada yake eneo la Kahororo na kuwa aliondoka Desemba 16 mwaka huu saa kumi jioni na kuaga kuwa anakwenda sokoni lakini hakurudi nyumbani.

“Baada ya dada yake kuona hakurudi, kesho yake ambayo ni Desemba 17, 2018 alianza kumtafuta hadi polisi bila mafanikio, lakini ilipofika saa 11:30 jioni aliamua kuongozana na mtu mwingine kwenda kwa hawala wa mdogo wake” alisema.

Alisema baada ya kufika huko ndipo aligundua kuwa mdogo wake ameuawa na kutoa taarifa polisi ambao waliwahi kufika katika eneo la tukio na kukuta marehemu hao na karatasi yenye maandishi hayo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.