AMUNIKE ATUA KAGERA KUSAKA VIPAJI

Na Allawi Kaboyo Bukoba.

Mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la mpira nchini (TFF) Ammy Ninje, amewataka vijana waliochaguliwa kujiunga na kambi itakayowezesha upatikanaji wa wachezaji wa kuongeza nguvu katika timu ya taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 17, kujiendeleza kielimu.

Ninje ametoa rai hiyo baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwachagua wachezaji 14 watakaokwenda kujumuika na wachezaji wengine wenye umri wa chini ya miaka 17, katika kambi itakayowekwa mkoani Arusha mwezi Aprili mwakani.

Amesema kuwa maisha ya mpira ni mafupi sana na kuwa wasiposoma sasa na kutegemea mpira pekee, siku za baadae watakuwa omba omba kutokana na kutokuwa na shughuli nyingine za kufanya, huku akisisitiza kuwa ambao hawako tayari kusoma hawatapata nafasi katika programu hiyo ambapo pia amewataka kuwa wakweli wakati wanapotakiwa kutoa taarifa zao hasa kuhusiana na umri.

“Unapokuwa mkweli unaepuka aibu ya kesho, unaweza kujiona kwa sasa uko salama lakini utapatikana tu, kuna kipimo cha MRI ukipigwa kwenye mwili wako utagundulika tu umri wako ni kiasi gani” amesema.

Kwa upande wake kocha mkuu wa timu ya taifa (Taifa stars) Emmanuel Amunike ambaye pia amehusika kuchagua wachezaji hao amebainisha kuwa kinachoangaliwa ni vipaji bila kujali mhusika kama anatoka familia yenye uwezo wa fedha au anatoka katika familia maskini.

Amunike amesema kuwa kila mmoja anapaswa kupata fursa ya kukua, na kuwa hilo ndilo analoliamini, huku akisisitiza kuwa wanapaswa kukua binafsi lakini pia wanapaswa kukua kama nchi.

Naye mkurugenzi wa kituo cha mpira wa miguu cha Karume Kids Sports Academy, Seif Mkude amesema kuwa amepata msukumo kuwaomba wataalam hao wa soka kufika mkoani Kagera kusaka vipaji, ili kuwawezesha vijana wa Kagera kupata fursa ambayo wamekuwa wakiikosa.

“Kagera tunakosa fursa nyingi za kimichezo kwa sababu tuko mbali, kwa hiyo wataalamu wengi wanapokuja wanaishia Dar-es-salaam au wakija kanda ya Ziwa wengi wanaishia Mwanza, kwa hiyo niliona nitumie fursa hii kuwaomba wafike huku maana kuna vipaji vingi vya mpira” amesema Mkude.

 

mwisho

 

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.