ALIYEWATAPELI WATALII DOLA 5000 AKAMATWA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inamshikilia Omwailimu Sosthenes ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Utalii ya  Arise Special Sunrise,kwa tuhuma za kuwatapeli watalii wawili Dola za kimalekani 5000.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, DCP Liberatus Sabas, amesema mtuhumiwa huyo aliwatapeli watalii hao ambaye mmoja anaishi Marekani na mwingine nchini India kwa makubaliano kwamba angewapeleka safari ambazo walizipanga.

Amesema baada ya mtuhumiwa huyo kuwatapeli wageni hao aliwatelekeza katika nyumba ya wageni maeneo ya Sinza na walipojaribu kuwasiliana naye aliwatolea lugha za vitisho hivyo kuamua kuripoti polisi.

“Sekta ya Utalii ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya serikali ambapo tunategemea itupatie fedha ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwahiyo watu kama hawa wanaofanya hivi wanalihujumu Taifa,” alisema DCP Sabas.

Kamanda Sabas amesema Mei 23, mwaka huu jeshi hilo liliwatia mbaroni watuhumiwa watano ambao wanatuhumiwa kuvunja nyumba na magodauni na kuiba katoni 500 za viatu zenye thamani ya Sh milioni 600.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Haruna Yusuph  (28) mkazi wa Makongo, Ally Bakari (53) wa Buza, Hawa Juma (32) mkazi wa Tabata  na wengine wawili kwamba walifanya wizi huo katika ghala la kampuni ya BataMei 21 mwaka huu saa 5:00 usiku.

“Watuhumiwa walikamatwa wakiwa na box saba za viatu, mabegi mawili ya viatu, pamoja na gari aina ya Mitsubishi Canter  T. 686 BWY ambalo lilitumika kubebea mizigo hiyo, katon 71 za bia, mifuko 18 ya sabuni ya unga na Injini 4 za Pikipiki, na mabalo 61 ya nguo za mitumba.

“Pia katika oparesheni nyingine iliyofanyika Julai 10 mwaka huu tulifanikiwa kukamata mtu mmoja (jina limehifadhiwa) eneo la Temeke Kisuma Bar ‘Sugar Ray’ akiwa na bastola moja aina ya Luger iliyotengenezwa Jamuhuri ya Czech yenye namba usajili A.368021,” alisema DCP Sabas.

Aidha amesema Juni 24, mwaka huu eneo la Kariakoo jeshi hilo lilimkamata mtuhumiwa Amin Kimaro (55) mkazi wa Manzese na wenzake watatu kwa kosa la wizi wa kughushi hundi za benki na kuziweka kwenye akaunti za washirika.

Amesema walipohojiwa walikiri kujihusisha na uhalifu huo kwamba walieleza kuwa wamekuwa wakighushi hundi za benki na kisha kuziweka katika akaunti ya benki ili kuiba fedha walizokusudia.

Pamoja na wahalifu hao, Jeshi la Polisi linashikilia gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 819 DED  waliyokuwa wakiitumia, simu za mkononi 8, kadi za simu 6 za mitandao mbalimbali, pamoja na deposit slip ya Sh milioni 1.973 ya hundi ya NMB kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kamanda Sabas amesema jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 12  wa wizi wa magari na pikipiki katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na mikoa jirani.

Amesema watuhumiwa hao walihojiwa na kukiri kuiba magari hayo ambayo baada ya kuyaiba huyauza katika mikoa mbalimbali na kwamba watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.