AKAMATWA KWA KUFANYA KAZI NCHINI BILA KIBALI.

 

Na,Allawi Kaboyo, Bukoba.

Raia wa Ufaransa Philippe Krynen anayefanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali la Patage Orphans Support amekamatwa na maafisa kazi mkoani Kagera, kwa tuhuma za kufanya kazi bila kibali.

Kukamatwa kwa Raia huyo ni mwendelezo wa zoezi la ukaguzi mahala pa kazi linaloendeshwa na maafisa kazi mkoani Kagera la kuhakikisha watu wote hasa Raia wa kigeni wanakuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Akiongelea zoezi hilo Afisa kazi mkoa wa Kagera Bi Hadija Hersi amezungumza kuwa wakati wakiendelea na ukaguzi wao katika taasisi mbalimbali, walibaini uwepo wa raia huyo ambaye amekuwa akifanya kazi kama meneja wa shirika hilo, na kuwatahadharisha raia wote wa kigeni kuhakikisha wanapata vibali kabla hawajaanza kufanya kazi hapa nchini.

”Kwasasa tunaendesha zoezi la kuwabaini wageni wanaofanya kazi bila vibali vya kufanya kazi na hapa tumebaini mgeni mmoja anayetambulika kwa jina la Philippe Krynen raia wa Ufaransa ambaye anafankisheriabila vibali, nitoe wito kwa wagaeni wote kuhakikisha wanafanya kazi wakiwa tayari wana vibali vya kuwaruhusu kufanya kazi tutakaowabaini wakiwa hawana vibali tutawachukulia hatua kali za kisheria” alisema afisa huyo.

Hata hivyo kukamatwa kwa raia huyo kukazua kutokuelewana baina ya wafanyakazi wa idara ya kazi na wafanyakazi wa shirika la Patage, huku Bi.Jean Mzena ambaye pia ni afisa kazi akiwaeleza watumishi wa shirika hilo waliokuwa wakilalamikia kukamatwa kwa kiongozi wao kuwa wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.

“Tumekuwa tukitumia ubinadamu tukimwambia kutafuta kibali mara nyingi na hajatii hivyo hutuwezi kuacha kutimiza wajibu wetu kisa ubinadamu, siwezi kuacha kufanya kazi yangu kisa ubinadamu ambavyo nikifukuzwa kazi watoto wangu wahangaike” alisema Bi. Jean Mzena.

Raia huyo amekabidhiwa mikononi mwa idara ya Uhamiaji mkoa wa Kagera kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

 

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.