Ripoti zinasema,wanafunzi wa chuo kikuu nchini Zimbabwe wameapa kutofanya mitihani yao hadi Rais Robert Mugabe atakapokuwa amejiuzulu.

Maelfu ya Wazimbabwe wametanda katika mitaa ya jiji la Harare tangu mapema wiki iliyopita kumshinikiza mkongwe huyo ajiuzulu, ambapo jana Jumapili mkongwe huyo alikataa kufanya hivyo katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni.
Ripoti mbalimbali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimesema wanafunzi hao “wamewafungia ndani wahadhiri wakikataa kufanya mitihani hadi Mugabe aondoke.”
Mugabe anakabiliwa na kitisho cha kushtakiwa na chama chake cha Zanu-PF ikiwa atashindwa kufanya hivyo leo.
Wanafunzi hao pia wametaka shahada ya umahiri (PhD) aliyotunukiwa Grace Mugabe ifutwe. Chuo Kikuu cha Zimbabwe kilimtunuku Grace shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika masuala ya malezi ya yatima mwaka 2014.
Chuo kimekataa kutoa maoni yoyote lakini chanzo kimoja kinasema kwamba mwanamama huyo alijiandikisha mwaka 2011 kwa ajili ya shahada ya uzamili lakini mkufunzi wake aliona “utafiti aliofanya ulikuwa wa ubunifu na wenye mchango mkubwa katika taaluma” kwa hiyo ukapandishwa hadhi na kuwa wa shahada ya uzamivu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.